Kwa mfano huu, ndivyo sisi mmoja mmoja tutakavyohesabiwa haki, TUKIJITAHIDI kumwiga Yesu kristo. Yehova Mungu atatuona 'watakatifu'.
Ukiweka lengo, naye atakupa NGUVU za kutimiza lengo lako.
Je, ni mambo gani machache tunayoweza kuyachukua kwa Yesu na kuanza kuyaiga?
1. UPENDO: Yesu alionyesha upendo kwa watu wote, waliomwamini na hata ambao hawakumwamini, waliokuwa wema kwake na waliokuwa adui zake, waliomtendea mazuri na waliomkosea pia. Petro alimkata mara tatu. lakini Yesu alifikiria sababu zilizomfanya Petro amkane, akawa mwenye KUKUBALI SABABU. Msongo/mkazo wa tukio la kuuwaw kwake, ulimfanya Petro amkane. yesu alimsamehe, na baadaye akaja kumpa madaraka makubwa sana!
SOMO LA KUIGA: Je, mimi/wewe hujitahidi kuelewa kwa nini 'mtu fulani' ametenda vile? Je, huwa tayari kumsamehe kwa moyo mmoja, hata kama hajaomba msamaha? Je, humsaidia ajitambue kosa lake kwa upendo? Je, huwa nia/unachagua watu wa kuwatendea mema na wengine unawabagua?Je, unaweka kinyongo mpaka kila ukimwona nyongo inamwagika? Kumbuka, tusipowasamehe watu makosa yao, Baba yetu wa Mbinguni hatatusamehe pia sisi makosa yetu. Mathayo 6:14,15.
2. UVUMILIVU: Yesu Kristo aliwavumilia sana wanafunzi wake. Mara kadhaa walibishana juu ya nani atakayekuwa mkuu/kiongozi kati yao Yesu akiondoka kurudi Mbinguni. Yesu aliwafundisha somo la UNYENYEKEVU kwa kuwaonyesha kwa vitendo. (a) Aliwaosha miguu yao akiwa amejishusha mno! (b) Alimweka mtoto mdogo mbele yao, na kuwaambia kwamba, mtu asipojinyenyekeza kama mtoto huyo, hawezi kurithi Ufalme. (c) Aliwaambia kwamba, mtu anayetaka kuwa mkubwa kati yao, awatumikie wengine na si kupiga ubwana juu yao. Petro alimwambia Yesu: “Bwana, je, wewe unaosha miguu yangu?” Yesu akamjibu: “Kile ninachofanya wewe hukielewi wakati wa sasa, bali utaelewa baada ya mambo haya.” Petro akamwambia: “Hakika wewe hutaosha kamwe miguu yangu.” Ona jinsi Petro alivyozungumza kwa mkazo, lakini akatenda kwa haraka-haraka. Yesu aliitikiaje?
Yesu akamjibu: “Isipokuwa nikuoshe, wewe huna sehemu pamoja na mimi.” Simoni Petro akamwambia: “Bwana, si miguu yangu tu, bali pia mikono yangu na kichwa changu.” Sasa Petro anapita mipaka! Lakini wakati wote watu walijua mtazamo wake. Hakuwa na hila.— Yohana 13:6-9.
3. BIDII YA KUHUBIRI NA KUFANYA WANAFUNZI: Je, tunamwachia mchungaji, mwinjilisti, au kiongozi yeyote kazi ya kuhubiri habari njema za Ufalme? Yesu alitembea nyumba kwa nyumba ili awapate watu wenye mwelekeo unaofaa kwa ajili ya Ufalme wa Yehova Mungu. Ndiyo kazi yake kubwa iliyomleta duniani. Alisema nendeni mkafanye wanafunzi toka mataifa yote.... Mathayo 28:19,20.
4. WATU WANAKUMBUKA NINI KUMHUSU YESU?
Huduma ya Yesu duniani ilikuwa ya miaka
mitatu na nusu tu. Lakini anakumbukwaje na wafuasi wake?
i. Je, alikuwa mtu
asiyefikika kwa sababu alikuwa mkamilifu na bila dhambi?
ii. Je, alipiga ubwana kwa
sababu alijua kwamba yeye ni Mwana wa Mungu?
iii. Je, aliwaogopesha au kuwalazimisha
wafuasi wake wamtii?
iv. Je, alifikiria sana jinsi alivyoonekana hivi kwamba hakuwa
mcheshi?
v. Je, alikuwa na shughuli nyingi sana hivi kwamba hakuwa na wakati kwa
walio dhaifu na wagonjwa, au watoto?
vi. Je, aliwadharau wanawake na watu wa jamii
zingine, kama ilivyokuwa kawaida ya wanaume wengi wakati huo? Tunajifunza nini
kutokana na mambo yaliyoandikwa kumhusu?
Yesu alipendezwa na watu. Tunapochunguza
huduma yake tunaona kwamba mara nyingi aliwaponya vilema na wagonjwa.
Alijitahidi sana kuwasaidia wenye uhitaji. Alipendezwa na watoto, naye
aliwaambia wanafunzi wake: “Waacheni watoto wachanga waje kwangu; msijaribu
kuwakomesha.” Kisha Yesu “akachukua watoto akawakumbatia na kuanza kuwabariki,
akiweka mikono yake juu yao.”
vii. Je, wewe hutafuta wakati wa kuwa pamoja na
watoto, au una shughuli nyingi sana hivi kwamba hata huwaoni? — Marko 10:13-16 ; Mathayo 19:13-15.
Yesu alipokuwa duniani, Wayahudi walikuwa
wamelemewa na amri na kanuni ambazo zilipita matakwa ya Sheria. Viongozi wao wa
kidini waliwatwika mizigo mizito, ambayo wao wenyewe hawakuisogeza kwa kimoja
cha vidole vyao. Mathayo 23:4 ; Luka 11:46. Yesu alikuwa tofauti sana. Alisema: “Njoni kwangu, nyinyi nyote mnaomenyeka na
kulemezwa mizigo, nami hakika nitawaburudisha nyinyi.”—Mathayo 11:28-30.
Watu waliburudika waliposhirikiana na Yesu.
Hakuwaogopesha wanafunzi wake wasiweze kujieleza. Kwa kweli, aliwauliza maswali
ili kuwatia moyo wajieleze. Marko 8:27-29. Inafaa waangalizi Wakristo wajiulize: ‘Je, waamini wenzangu wananiona hivyo?
Je, kweli wazee wengine hunieleza maoni yao, au
husita kufanya hivyo?’ Inaburudisha kama nini waangalizi wanapokuwa wenye
kufikika, wenye kuwasikiliza wengine, na wasio wagumu! Kukosa busara huwavunja
wengine moyo wasizungumze kwa uhuru na kwa wazi.
Ingawa Yesu ni Mwana wa Mungu, hakutumia
vibaya uwezo wala mamlaka yake. Lakini alijadiliana na wasikilizaji wake.
Ilikuwa hivyo Mafarisayo walipojaribu kumnasa kwa swali hili la hila: “Je,
yaruhusika kisheria kumlipa Kaisari kodi ya kichwa au la?” Yesu aliwaambia
wamwonyeshe sarafu naye akawauliza: “Sanamu na mwandiko huu ni wa nani?”
Wakasema, “Wa Kaisari.” Ndipo akawaambia: “Basi, mlipeni Kaisari vitu vya
Kaisari, lakini mlipeni Mungu vitu vya Mungu.” (Mathayo 22:15-21)
Alihitaji tu kujadiliana nao kwa akili ili kujibu swali lao.
Je, Yesu alikuwa mcheshi? Huenda wasomaji
wengine wakaona ucheshi wa aina fulani wanaposoma mahali ambapo Yesu alisema
kwamba ni rahisi zaidi ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko mtu tajiri
kuingia katika Ufalme wa Mungu. (Mathayo 19:23, 24)
Wazo lenyewe la ngamia kujaribu kupita katika tundu la sindano halisi ya
kushona limetiwa chumvi. Mfano mwingine wa utiaji chumvi ni ule wa kuona unyasi
katika jicho la ndugu na usione boriti katika jicho lako mwenyewe. (Luka 6:41, 42)
Kwa kweli, Yesu hakuwa mshauri mkali bali alikuwa mchangamfu na mwenye urafiki.
Kwa Wakristo leo, ucheshi unaweza kupunguza huzuni wakati wa msiba.
Yesu Aliwahurumia Wanawake
Wanawake walihisije walipokuwa na Yesu?
Bila shaka, Yesu alikuwa na wafuasi wengi wanawake waliokuwa waaminifu,
waliotia ndani Maria, mama yake. (Luka 8:1-3; 23:55, 56; 24:9, 10)
Wanawake walijihisi huru kumwendea Yesu hivi kwamba pindi moja mwanamke fulani
‘aliyejulikana kuwa mtenda-dhambi’ alimwosha miguu kwa machozi na kuipaka
mafuta yenye marashi. (Luka 7:37, 38)
Mwanamke mwingine aliyetokwa damu kwa miaka mingi, alijikakamua kupita katikati
ya watu ili kugusa vazi lake na kuponywa. Yesu alisifu imani yake. (Mathayo 9:20-22)
Naam, wanawake walimwona Yesu kuwa mwenye kufikika.
Pindi nyingine, Yesu alizungumza na
mwanamke Msamaria kwenye kisima. Alishangaa sana na kusema: “Ni jinsi gani
kwamba wewe, ujapokuwa Myahudi, waniomba mimi kinywaji, wakati mimi ni mwanamke
Msamaria?” Wayahudi hawakuwa na shughuli na Wasamaria. Yesu alimfunza kweli
nzuri kuhusu ‘maji yanayobubujika ili kutoa uhai udumuo milele.’ Alistarehe
kabisa kati ya wanawake. Hakuhisi kwamba kuongea na wanawake
kulimshushia heshima.—Yohana 4:7-15.
Yesu anakumbukwa kwa sifa ya huruma, kutia
ndani roho yake ya kujidhabihu. Alikuwa mfano halisi wa upendo wa kimungu. Yesu
anaweka kiwango cha kufuatwa na wote wanaotaka kuwa wafuasi wake. Wewe unafuata
kwa ukaribu jinsi gani kielelezo chake?—1 Wakorintho
13:4-8; 1 Petro
2:21.